Saturday, August 8, 2015

Simba: Magufuli Ikulu ni lazima

MWENYEKITI wa Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT), Sophia Simba amesema jumuiya hiyo ya wanawake wa CCM, imejipanga kuhakikisha mgombea urais wa chama hicho, Dk John Magufuli anashinda katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 25 mwaka huu.
“UWT tumejipanga kama mnavyojua sisi ni jeshi kubwa na tutahakikisha tunampeleka Magufuli Ikulu... Leo (jana) tuna kikao kizito sana cha kuweka mikakati ya kumpeleka Magufuli Ikulu,” alisema Simba jana mkoani hapa. Tayari UWT imeshatoa kaulimbiu katika uchaguzi huo, inayosema ‘Wanawake jeshi kubwa, Magufuli Ikulu ni lazima’.


Kwa sasa Magufuli, Waziri wa Ujenzi mwenye sifa ya uadilifu katika kusimamia miradi mikubwa ya miundombinu nchi nzima, anatarajiwa kuanza kuzunguka nchi nzima kusaka wadhamini, baada ya kukabidhiwa fomu ya kuwania urais na Tume ya Taifa ya Uchaguzi.
Akijibu swali kuhusu madai kuwa anatarajiwa kuhama chama hicho na kujiunga na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kumfuata mgombea urais wa CCM aliyeenguliwa katika vikao vya mchujo, Edward Lowassa, Simba alisema minong’ono hiyo haina ukweli.
“Hayo ni mawazo tu, huwezi kumzuia mtu kuwaza, lakini mimi niliingia CCM kwa sababu zangu na sina sababu yoyote ya kuondoka CCM, maana ndicho kimenilea na kunikuza. “Kama Lowassa amehama chama ana sababu zake, mimi sina sababu yoyote ya kufanya hiyo. Tulikuwa na timu sasa tumevunja imebaki timu moja tu Magufuli ambayo ni kambi ya CCM,” alisema Simba.
Aidha alisema hakuna mpasuko wowote ndani ya CCM kutokana na kuondoka Lowassa, kwani pamoja na kuhama kwa baadhi ya wanachama waliofananishwa na oili chafu, CCM bado ina mamilioni ya wanachama. Alisema wanaodai kuna mmomonyoko kwa kuondoka Lowassa CCM siyo kweli na hizo ni propaganda za kisiasa lakini kimsingi hakuna mmomonyoko wowote.
“CCM hatutishiwi nyau, uwezo wetu ni mkubwa.” Simba, ambaye pia ni Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto, alikuwa amevalia dera lililoandikwa ‘Baki njia kuu, mchepuko siyo dili’.
Alisema mchakato ndani ya CCM wa kumpata mgombea urais umeshamalizika na makundi yote yamekwisha, limebaki moja la Magufuli ambalo ni kundi la CCM.

No comments:

Post a Comment