Saturday, August 8, 2015

Simba: Magufuli Ikulu ni lazima

MWENYEKITI wa Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT), Sophia Simba amesema jumuiya hiyo ya wanawake wa CCM, imejipanga kuhakikisha mgombea urais wa chama hicho, Dk John Magufuli anashinda katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 25 mwaka huu.
“UWT tumejipanga kama mnavyojua sisi ni jeshi kubwa na tutahakikisha tunampeleka Magufuli Ikulu... Leo (jana) tuna kikao kizito sana cha kuweka mikakati ya kumpeleka Magufuli Ikulu,” alisema Simba jana mkoani hapa. Tayari UWT imeshatoa kaulimbiu katika uchaguzi huo, inayosema ‘Wanawake jeshi kubwa, Magufuli Ikulu ni lazima’.

Maalim Seif awatisha wafuasi wa Lipumba

WAFUASI wa aliyekuwa Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF) na pia mwenyekiti mwenza wa muungano wa wapinzani wanaounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), Profesa Ibrahim Lipumba, wameanza kushughulikiwa na kutakiwa kuchagua moja; kuendelea kuwa ndani ya chama hicho au kutoka.
Ingawa Profesa Lipumba alipojiuzulu uenyekiti, alisema ataendelea kuwa mwanachama wa CUF, lakini Katibu Mkuu wa chama hicho, Maalim Seif Sharif Hamad amewataka wanachama waliokuwa wakimuunga mkono, kuamua moja, kubaki ndani ya chama hicho kama alivyoamua mchumi huyo mashuhuri duniani, au kutoka.