Thursday, June 7, 2012

 

CHADEMA yamlilia Mbunge wa CUF


na Abdallah Khamis, Lindi

MBUNGE wa Lindi Mjini, Salum Barwani, ametakiwa kuachana na Chama cha Wananchi (CUF) na badala yake ajiunge na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) ili aweze kuwatumikia wananchi ipasavyo.
Kauli hiyo ilitolewa jana na Mwenyekiti wa Taifa wa CHADEMA, Freeman Mbowe wakati akijibu kero mbalimbali za wananchi wa Kata ya Ng’apa katika Jimbo la Lindi Mjini na kusema ndani ya CUF, Barwan ataendelea kuwa mtumwa wa maamuzi ya viongozi wake pasipo kuwatumikia wananchi.
Maamuzi ya Mbowe kumkaribisha Barwan, yalitokana na malalamiko ya wananchi kuwa jitihada za mbunge huyo kuwatumikia zinakwamishwa na viongozi wa serikali pamoja na madiwani wa mkoa huo, na kwamba viongozi wa CUF Taifa wanashindwa kumsaidia katika vita hiyo.
Mbowe alisema katika mazingira ya CUF, Barwan ataendelea kutaabika kwa kuwa viongozi wake wa kitaifa wameamua kumsusa kwa kufunga ndoa na Serikali ya CCM, hivyo hatoweza kusimamia maslahi ya wananchi.
“Sina ugomvi na Barwan, tunafanya nae kazi vizuri ila misimamo ya viongozi wake wakuu ni tatizo kwake, ninamshauri ajitathmini, na huku kwetu mlango uko wazi, anaweza kuusukuma na kuingia kwa ajili ya kuwatetea wana Lindi,” alisema Mbowe.
Kauli hiyo ilionekana kumchoma aliyekuwa mpiga debe wa mbunge huyo, Abdallah Madebe, ambaye alikiri kuwa hatima ya CUF haieleweki na hataki chama hicho kimfie mikononi.
Kutokana na hilo, Madebe aliamua kujiondoa katika chama hicho na kutangaza kujiunga na CHADEMA, hivyo kupokelewa rasmi na Mbowe.
Malalamiko mengine ya wananchi hao yalikuwa katika suala zima la mfumuko wa bei, kukosa huduma za afya na wanafunzi kutozwa shilingi 20,000, kwa ajili ya ulinzi wa shule za serikali.
Mkazi wa Ng’apa, Rashid Issa ‘Mbele wapi’, alisema hawajui hatma ya nchi yao kwa kuwa na maisha yao kutokana na mfumuko wa bei unaojitokeza kila wakati, huku wakiendelea kutozwa kodi katika vivuko vya mazao na fedha hizo kuishia mikononi mwa wajanja.
Akijibu hoja hizo, Mbowe alisema maisha magumu kwa Watanzania ni matokeo ya sera mbovu za Serikali ya CCM juu ya kusimmia uchumi wa nchi.
Kuhusu matatizo ya wananchi, Mbowe aliwataka wakazi wa Lindi kutowavumilia viongozi wazembe ambao hawawezi kuwaelezea kodi zao zilivyotumika wakati wao wanashindwa kupata huduma za msingi.
Dk. Slaa awavaa askari uwanjani
Akizungumza katika mkutano uliofanyika katika Uwanja wa Ilulu mkoani hapa, Katibu Mkuu wa CHADEMA, Dk. Willbroad Slaa aliwataka askari polisi wasipate tabu ya kurekodi mikutano yao bali fedha wanazonunulia kanda za kurekodia wazitumie kuboreshea maisha yao.
Alisema katika mikutano ya CHADEMA, askari wanajaa kwa wingi kwa lengo la kusikiliza vitu gani vinaongelewa ili wawafikishie mabosi wao, ambao hawawajali kimaslahi na kuwaacha wakiendelea kutaabika kwa hali ngumu, huku wengine wakiendelea kukaa katika nyumba za bati maarufu kama ‘full suti’.
“Ninyi maaskari mnanishangaza sana, ufisadi umejaa kila sehemu, badala ya kushughulika na hayo, ninyi mnakuja kurekodi ili mseme tunachochea vurugu, sasa ninawaambia nina barua ya viongozi wenu kwenda kwa rais, ikimlalamikia RPC aliyeondoka wa mkoa huu kwa kufanya ufisadi wa milioni 34 kisha akaondoka kabla ya kuchukuliwa hatua,” alisema Dk. Slaa.
Alisema atakachoweza kuwasaidia askari ni kuhakikisha kuwa mishahara yao inaongezwa baada ya mwezi wa saba, vinginevyo Rais Kikwete ajiandae kwa kuipokea nguvu ya umma kwa ajili ya kudai maslahi ya walimu na askari pamoja n watumishi wengine.
Dk. Slaa alisema kama kuna watu wanaostahili kukamatwa au kufuatiliwa, ni Mkuu wa Polisi nchini pamoja na Waziri Khamis Kagasheki ambaye kwa sasa ni Waziri wa Maliasili na Utalii, kwa kuwa waliamua kuwatisha askari wakati walipodai fedha kiasi cha shilingi laki moja na nusu baada ya kutangaziwa bungeni kuwa fedha hizo zipo katika resheni yao.
Lema amuonya Membe asiwazie urais
Aliyekuwa Mbunge wa Arusha Mjini, Godbles Lema akizungumza katika mkutano huo, alisema Waziri wa Mambo ya Nje na Mahusiano ya Kimataifa, Bernad Membe, amepoteza sifa ya kufikiria kuwa kiongozi wa nchi kutokana na kushindwa kuusaidia Mkoa wa Lindi kuondokana na umaskini unaoukabili.
Alisema kama Membe angekuwa kiongozi makini, angetumia fursa yake ya kusafiri nje kila wakati kutangaza vivutio vya Mkoa wa Lindi na kuufanya uwe wa kitalii kama mikoa mingine inayosifika kwa utalii Tanzania.
Mnyika awashtukia wabunge wa CCM
Mbunge wa Ubungo, John Mnyika alisema kama Rais Kikwete asipopeleka bajeti yenye kupunguza mfumuko wa bei katika Bunge lijalo, CHADEMA itahamasisha nguvu ya umma kumshinikiza afanye hivyo.
Alisema hata kauli inayotolewa na wabunge wa CCM kuwa wataigomea bajeti ijayo ni ya kujikosha mbele ya jamii, kwa kuwa wanajua wazi suala hilo haliwezekani kulingana na katiba waliyo nayo.
“Hawa wanasema wataipinga bajeti wakati wana hamu ya kupokea posho za bungeni, mbona wanajidanganya kwa kuwa wakifanya hivyo rais atavunja Bunge, na kwa hofu ya matendo yao wengi wanajua hawataweza kurudi, hivyo hizo ni propaganda tu,” alisema Mnyika.
Sugu aapa kulia na ajira za vijana
Mbunge wa Mbeya Mjini, Joseph Mbilinyi, alisema wakati anaelekea Mtwara akiwa ndani ya ndege, alijua mikoa hiyo ya kusini ni ya kupigiwa mfano kutokana na aina ya watu aliokuwa nao katika ndege, kwamba hata vijana wa Mkoa wa Lindi watakuwa wananufaika na rasilimali za mkoa huo.
“Nilipotua nikawauliza kama vijana wananufaika na gesi inayopatikana katika mikoa yenu, cha ajabu mnaniambia kuwa mnachopata ni vifaa vya kukingia vichwa na hamruhusiwi kuingia hata katika maeneo ya wawekezaji kufanya kazi, hili nitakufa nalo bungeni,” alisema Sugu.
Mwenyekiti wa Kijiji avua gamba na kuvaa gwanda
Mwenyekiti wa Serikali ya Kijiji cha Mbanja mkoani Lindi, Issa Selemani, ameachia nafasi hiyo na kujiunga na CHADEMA, huku akisema anatafuta haki ya watu wote badala ya kusimamia maslahi ya wachache.

No comments:

Post a Comment