Sunday, February 17, 2013




Padre E. Mushi Paroko wa parokia ya Minara Miwili Mtoni Zanzibar ameuawa kwa kupigwa risasi na watu wasiofahamika asubuhi hii.

Ameuawa wakati akijiandaa kuingia kanisani akitokea kwenye gari yake ambapo ghafla ilitokea gari ndogo na waliokuwamo ndani ya gari ile wakamrushia risasi.

Kwa siku za hivi karibuni kumekuwako na vitisho vya wazi wazi dhidi ya wakristu huko visiwani Zanzibar ambapo inaelezwa kuwa jeshi la polisi halijafanya juhudi yoyote kuzuia tishio hili. Kumekuwapo na vipeperushi vinavyodai kuwa kupigwa risasi kwa padre Ambrose sio mwisho wa mapambano. 

PADRI APIGWA RISASI USIKU HUU VISIWANI ZANZIBAR

 

Padre Ambros Mkenda wa Zanzibar apigwa risasi


 Picture

Father Ambros Mkenda wa Kanisa la Katoliki la Mpendae amepigwa risasi na watu wasiojulikana nje ya nyumba yake majira ya saa 12 jioni leo wakati akitokea kanisani. Kamanda wa polisi wa Mkoa wa Mjini Magharibi Azizi Juma amethibisha kutokea kwa tukio hilo na amesema hakuna mtu anayeshikiliwa kuhusika na tukio hilo lakini uchunguzi unaendelea. Father Mkenda hivi sasa anapatiwa matibabu katika hospitali ya Mnazi Mmoja, ambapo Askofu wa Anglikan Michael Hafidh amesema bado ni mapema mno kuelezea kama ataendelea kuwepo hospitalini hapo au atasafirishwa huku akilaani vitendo ambavyo hivi vinavyoendelea vya kuwahujumu viongozi wa dini. (picha: Salma Said)
Watu wasiojulikana leo wamempiga risasi Father, Ambros Mkenda wa Kanisa Katoliki la Mpendae Mjini Zanzibar nje ya nyumba yake majira ya saa 12 jioni wakati akitokea Kanisani.

Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Mjini Magharibi Aziz Juma Mohammed amethibitisha kutokea kwa tukio hilo ambalo alisema Father amepigwa risasi na ameumizwa sehemu ya kichwa na amekuwa akitoka damu nyingi kichwani na tayari anapatiwa matibabu katika hospitali kuu ya Mnazi Mmoja.
Alisema jeshi la polisi linaendelea na uchunguzi wa tukio hilo ili kubaini wahusika walifanya uhalifu huo kwa madhumuni gani kabla ya kuchukuliwa hatua za kisheria.
“Sisi tunahesabu kuwa kitendo hiki ni kitendo cha kihalifu na tunawatafuta wahalifu waliofanya kitendo hiki kwa hivyo bado ni mapema kusema kwamba kitendo hiki kimefanywa na nani kwa kuwa bado uchunguzi wetu unaendelea na hadi sasa hakuna mtu tuliyemshika kuhusikana na tukio hili” alisema Kamanda.
Kamanda Aziz akisimulia tukio hilo alisema walipata taarifa majira ya saa 2 na kwenda katika eneo la tukio ambapo Father alikuwa akitokea kanisani na kutaka kuelekea nyumbani kwake wakati akiwa ndani ya gari ndipo aliposhambuliwa na watu wasiojulikana na kuanguka.
“Tumekuta mabaki ya risasi ndani ya gari yake na katika vioo vyake vya gari vimevunjika na tumekuta damu chini pale” alisema Kamanda.
Aidha Kamanda Azizi alisema Father Ambros yeye ni mhasibu pale kanisani na hivyo mara nyingi watu wananaamini kwamba katika siku za krismass mara nyingi sadaka hukusanywa fedha nyingi na hivyo wanamini kwamba alikuwa fedha mikononi na ndipo inawezekana waliamua kumpiga risasi wakitaka kuchukua fedha hizo.
Hata hivyo alisema uchunguzi wa awali ndio utakaoeleza ni suala gani lililopelekea kupigwa risasi lakini wanaendelea na uchunguzi huo ambapo uchunguzi ndio utakaojulikana sababu kamili ya tukio hilo.
Akizungumzia tukio hilo, Askofu Michael Hafidh wa Kanisa la Anglikan la Mkunazini amesema wamesikitishwa na wamepokea kwa mshituko mkubwa tukio hilo hasa kwa kuzingatia matukio kama hayo hayajawahi kutokea ya kuwahujumu viongozi wa dini.
Alisema tukio hilo ni miongoni mwa matukio ya kushtusha na yanaashiria hali mbaya ya kiusalama na kuwaomba viongozi wa serikali kuchukua hatua za tahadhari kubwa kwani matukio kama hayo yameanza kutokea kwa viongozi wa dini ambapo mwanzo ilianzia kwa Sheikh Soraga na baadae kutokea kwa Father Ambros.
“Hii ni hali ya hatari katika nchi yetu na haipendezi lakini serikali lazima ijue sisi hatuwezi kujua wala hatuwezi kujilinda lakini serikali inapaswa kutulinda sisi ndio wananchi wake” alisema Askofu Hafidh.
Askofu Hafidh alisema hivi karibuni kumekuwepo vipeperushi vilivyosambazwa na watu vikiwatisha watu wenye imani ya kikristo ambapo alisema miongoni mwao walikuwa na khofu juu ya kusambazwa kwa vipeperushi hivyo na kuiomba serikali iongeze ulinzi.
“Tumeona hivi vipeperushi na kwa kweli tulikuwa na khofu juu ya vipeperushi hivi lakini ndio tunasema tunaelekea wapi katika maisha haya,” alisema Akofu Hafidh.
“Sisi hatuamini kwamba kuna kisasi kwa viongozi wa dini lakini tunachukulia hilo ni tukio la kihalifu na pia hatuna vipeperushi vya aina yoyote vinavyoelezea kuwatisha viongozi wa dini kwa hivyo tunachukulia hayo ni matukio ya kihalifu na wala hatuamini kwamba matukio haya ni ya dini fulani,” alisema Kamanda Azizi.
Akielezea kuhusiana na hilo Kamanda Aziz alisema jeshi la polisi limejipanga na kuzidisha ulinzi katika maeneo yote ya makanisa ambapo kumesambazwa polisi wa kutosha kwa kuwa wanajua wakati wa sherehe mambo ya kihalifu hujitokeza.
“Sisi kawaida huwa tunaweka ulinzi siku za sherehe zozote lakini kwanza makanisa yote yamewekwa ulinzi wa kutosha kabisa lakini wahalifu wanapotaka kufanya uhalifu huwezi kujua watatumia mbinu gani na saa ngapi na watafanya uhalifu huo wapi, lakini ulinzi upo wa kutosha,” alisisitiza Kamanda Aziz.

Spika akaliwa kooni

Spika akaliwa kooni


Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kimetangaza kwenda kwa wananchi ambao wanaunda mahakama iliyo kubwa kuliko zote nchini kwa nia ya kuwapelekea hoja binafsi zenye maslahi kwa taifa zilizozimwa nje ya utaratibu na kiti cha Spika.

Aidha, Chadema kimewaelekeza wabunge wake wote watakaoitwa na Kamati ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge, wasiende kuhojiwa kama alivyoelekeza Spika wa Bunge, Anne Makinda.

Msimamo huo ulitangazwa jana jijini Dar es Salaam na Katibu Mkuu wa Chadema, Dk. Willibrod Slaa, kwa waandishi wa habari na kufafanua kuwa wabunge wa chama chake wameelekezwa wasiende kuhojiwa kutokana na kiti cha Spika kuonyesha upendeleo wa wazi kwa serikali dhidi ya hoja binafsi za wabunge.

Hoja zilizokataliwa ni ya Mbunge wa Kuteuliwa, James Mbatia kuhusu udhaifu katika mitaala na hoja ya Mbunge wa Ubungo (Chadema), John Mnyika, iliyohusu matatizo ya maji katika Jiji la Dar es Salaam.

Hoja ya Mbatia ilikataliwa Ijumaa iliyopita na kuwalazimisha wabunge wote wa upinzani kutoka nje ya ukumbi wa Bunge wakati hoja ya Mnyika ilikataliwa juzi na kusababisha mvutano bungeni kati ya serikali na wabunge wa CCM kwa upande mmoja na wale wa upinzani kwa upande mwingine na kumlazimisha Naibu Spika Ndugai, kuahirisha kikao.

Dk. Slaa alisema wabunge wa Chadema wametakiwa kutoitikia wito wa kuhojiwa na Kamati hiyo inayoongozwa na Mbunge wa Mlalo (CCM), Brigedia Jenerali mstaafu Hassan Ngwilizi, hadi pale rufaa 10 zilizokatwa na wabunge wa Chadema kwa nyakati tofauti zitakapotolewa maamuzi.

KWENDA KWA WANANCHI
Akizungumzia suala la kwenda kwa wananchi, Dk. Slaa alisema kuwa hatua hiyo imechukuliwa na chama hicho baada ya kuona kwamba Bunge ambalo ni chombo pekee kikuu nchini kwa mujibu wa Ibara ya 63 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania chenye wajibu wa kuisimamia serikali kugeuzwa na viongozi wake kuwa sehemu ya serikali.

“Na ndiyo maana unaona sasa Spika anatumika kupindisha kanuni za Bunge kwa minajili ya kutimiza matakwa ya serikali na hivyo kuonyesha kwamba yupo pale kwa manufaa ya serikali kinyume cha kanuni ya nane ya Bunge,” alisema.

Alisema Chadema kama chama makini, hakiwezi kukaa kimya na kuona Bunge ambalo ndilo chombo kitakatifu zaidi hata ya Ikulu kwa sababu linawakilisha wananchi, linageuzwa kuwa ‘komedi’ kwa kuzima hoja binafsi za wabunge kama ya Mnyika na Mbatia na hivyo kufanya Bunge kutokuwa na tija, zaidi ya kuteketeza mamilioni ya fedha za wananchi.

Alisema Mkutano wa Bunge unaoendelea sasa unagharimu zaidi ya Shilingi bilioni moja na  alitarajia fedha hizo zitumike kuhalalisha mijadala na maamuzi yenye tija tofauti ilivyofanyika safari hii.

Akizungumzia uamuzi wa kuwazuia wabunge wao kutoitikia wito wa kamati ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge, kama kilivyoelekeza kiti cha Spika mpaka pale maamuzi ya rufaa zote kumi zilizokatwa na wabunge wa chama chake zilizoko kwa Spika yatakapotolewa bungeni na tena hadharani.

  Dk. Slaa alisema wamefikia hatua hiyo kwa misingi kuwa Spika ambaye anayepaswa kusimamia kanuni, ndiye amekuwa wa kwanza kuzivunja.

“Kati ya rufaa hizo kumi alizozikalia Spika, nitaje mbili kwa faida ya wananchi, moja ni ile ya Godbless Lema (Mbunge wa Arusha Mjini (Chadema) aliyetakiwa kuthibitisha tuhuma kwamba Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, alilidanganya Bunge na alipeleka ushahidi na Spika akaukalia hadi leo,” alisema.

Dk. Slaa alitaja pia ushahidi alioutoa Mbunge wa Singida Mashariki (Chadema), Tundu Lissu, kuhusiana na tuhuma za kuteuliwa majaji wasio na sifa na alithibitisha kwa vielelezo alivyovipeleka kwa Spika ikiwa ni pamoja na kumtaja jina jaji mmoja wa Mahakama ya Rufaa, lakini juhudi zake zote zimeishia kwenye mikono ya Spika.

Dk. Slaa aliwaasa Watanzania wanapokwenda kwenye mabaraza ya katiba kuhakikisha wanajenga hoja zitakazozuia Spika kupatikana kutoka kwenye chama cha siasa, badala yake wapendekeze Spika kupatikana kutokana na sifa maalum kama za elimu na kupitia kwenye uhakiki wa chombo maalum kitakachopendekezwa kwa ajili ya kufanya kazi hiyo.


NGWILIZI AKABIDHIWA JUKUMU
Kamati  ya Uongozi ya Bunge imepeleka sakata la vurugu zilizotokea juzi jioni katika Kamati ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge, ili ilichunguze na kutoa mapendekezo bungeni kabla ya Mkutano wa 10 kumalizika.

Aidha, kamati hiyo imesimamisha uwasilishaji wa hoja binafsi zilizopangwa kuwasilishwa na wabunge katika mkutano huu.

Vurugu hizo zilitokea juzi baada ya Waziri wa Maji, Profesa Jumanne Maghembe, kuwasilisha hoja ya kutaka hoja ya Mnyika iondolewe.

Akizungumza mara baada ya kipindi cha maswali na majibu bungeni jana, Spika Makinda, alisema maamuzi hayo yalifikiwa juzi katika kikao cha dharura cha kamati ya Uongozi.
“Kamati ilikubaliana kuwa hoja zote binafsi za wabunge zisiwasilishwe bungeni kutokana na utovu wa nidhamu uliokuwa umeanza ili kuzuia mwendelezo ambao ungeweza kujitokeza katika hoja binafsi zilizobakia kwa kulinda heshima ya Bunge,” alisema na kuongeza:

“Kamati ilikemea kwa nguvu zote vitendo hivyo na kubainisha kwamba endapo vitaachiwa viendelee vinaweza kusababisha madhara makubwa kama kupigana ndani ya Bunge.”

Kuhusu uamuzi wa kusitisha hoja binafsi, Spika Makinda alisema imelazimu Bunge  kuahirisha mijadala ya Hoja Binafsi kutokana na tabia iliyojitokeza ya utovu wa nidhamu kwa baadhi ya Wabunge.

Alisema wabunge hao waliamua  kwa makusudi kuanzisha vurugu na hivyo kulifanya Bunge lianze kupoteza heshima yake ya Kibunge.

“Waheshimiwa wabunge, siku zote nimekuwa nikisisitiza matumizi ya Kanuni za Bunge ambazo ndizo mwongozo wa uendeshaji wa Bunge.  Hoja Binafsi za wabunge zinaongozwa na Kanuni za Bunge kuanzia Kanuni ya 53 hadi 58 na Kanuni za majadiliano zinaongozwa na Kanuni kuanzia 59 hadi 71 ambazo kwa ujumla wake zikifuatwa kama inavyotakiwa, vurugu haiwezi kutokea Bungeni,” alisema.

Alisema katika mkutano huu ambao unatarajiwa kumalizika Ijumaa,  imeonyesha waziwazi baadhi ya wabunge kwa makusudi na kwa nia ya kupotosha wananchi wakitumia vibaya kanuni hizo na wakati mwingine kuwadanganya wananchi ambao kwa bahati mbaya hawazifahamu kanuni au hazifuatwi na kiti ama zinakiukwa.

“Waheshimiwa Wabunge, kwa masikitiko makubwa sote tulishuhudia vurugu zilizojitokeza katika Bunge hili hasa wakati wa mjadala wa hoja binafsi za wabunge, kimsingi huu ulikuwa ni utovu wa nidhamu wa hali ya juu kutokea katika Historia ya Bunge letu,” alisema na kuongeza:

“Taasisi ya Bunge inalaani vitendo vilivyojitokeza jana (juzi) vilivyovunja Kanuni ya 60(2) inayokataza Mbunge kuzungumza kabla ya kuruhusiwa na Spika na Kanuni ya 60(12) inayowataka Wabunge kukaa chini wakati wowote Spika anaposimama kutaka kuzungumza.”
Aidha, alisema kumekuwa kuna madai kuwa Kiti kinatoa upendeleo wa wazi kwa Serikali dhidi ya Upinzani, jambo ambalo si kweli.

Hata hivyo, alisema  kama maamuzi yanayofanywa na Kiti yana kasoro kanuni zinaruhusu mbunge ambaye hakuridhika na maamuzi hayo, kukata rufaa kwenye Kamati ya Kanuni za Bunge kwa mujibu wa Kanuni ya 5 (4).

Alisema  vitendo vya uvunjifu wa Kanuni na kusababisha fujo kumedhalilisha Kiti na Taasisi ya Bunge kwa ujumla.

Akizungumzia kuhusiana na kuondolewa kwa hoja ya Mnyika, Makinda alisema hoja hiyo ilikidhi vigezo na alipewa nafasi ya kuiwasilisha Bungeni na akawasilisha hoja yake.
Alisema baada ya Hoja hiyo kuwasilishwa, kwa mujibu wa kanuni ya 53(6) (c) Waziri wa Maji ambaye ndiye msemaji wa Serikali kuhusu maudhui ya Hoja husika, alipewa nafasi ya kuwa mchangiaji wa kwanza na kutoa maoni ya shughuli za Serikali juu ya hoja ya Mnyika.

‘KITI CHA SPIKA KINAYUMBA’
Baadhi ya watu wamesema Spika Makinda na Naibu wake. Job Ndugai  ndiyo chanzo cha kuvuruga Bunge na kusababisha heshima yake kushuka mbele ya Watanzania.

DEUS KIBAMBA
Mwenyekiti wa Jukwaa la Katiba Tanzania, Deus Kibamba, alimkumbuka Spika aliyepita, Samel Sitta, na kusema kuwa alikuwa anatenda haki na ndiyo maana wabunge wengi walikuwa wanamheshimu na hapakuwa na vurugu kama za sasa.

Alisema ili kulipa Bunge heshima yake inayostahili, ni lazima kila hoja binafsi inayowasilishwa iheshimiwe na mbunge aliyeiwasilisha apewe heshima yake.

Alimtaka Spika kuacha utaratibu wa kufanya kazi kwa kuangalia itikadi za chama.
Alisema hoja za wapinzani ambazo wamekuwa wakiziwasilisha bungeni zimekuwa na maana, lakini wabunge wa CCM pamoja na Spika wamekuwa wakiziponda bila sababu na kutaka ziondolewe mezani.

“Hoja hizi za wapinzani zimekuwa zikiwapa changamoto wabunge wa CCM,  ingawa wamekuwa wakiziona kama hazina maana,” alisema Kibamba.
RAIS TLS

Rais wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS), Francis Sitolla, alisema kuna udhaifu mkubwa katika kuwadhibiti wabunge na kuwaelekeza wanapokuwa wanajadili hoja mbalimbali.
Alisema ni dhahiri kwamba kiti cha Spika kinayumba kutokana na kuonekana wazi kwamba anaendesha Bunge kwa upendeleo huku akiwanyima wapinzani haki.

Aliongeza kuwa kiti cha Spika kama mwamuzi huru, kinatakiwa kutenda haki kwa kila upande ili jamii na wabunge waweze kukiamini hususani inapozuka mijadala mikali.

Alisema matatizo ya kumchagua Spika anayetokana na chama cha siasa kwa sasa yameanza kujitokeza na kwamba hali hiyo inaweza kuwa mbaya katika kipindi kilichobaki kabla ya Uchaguzi Mkuu mwaka 2015.

Aidha, Stolla aliwataka wabunge kwa upande mwingine kuwa wavumilivu pale hoja zinapojadiliwa, lakini alisema hilo litaweza kufanyika kama wataamini wanatendewa haki ndani ya Bunge.

“Spika siyo tu aonekane ametenda haki kwa wabunge wa upinzani bali haki lazima ionekane imetendeka na hapo ndipo anaweza kuaminiwa na pande zote,” alisema Stolla.

HELLEN KIJO-BISIMBA

Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu, Dk. Hellen Kijo-Bisimba, alisema vurugu za juzi bungeni zilitokana na kiti cha Spika kuvaa miwani ya kuona upande mmoja na  kwamba huo ni udhaifu mkubwa.

Dk. Bisimba alisema Bunge limeshindwa kuangalia shida mbalimbali zinazowakabili Watanzania badala yake limejikita kukwamisha hoja za wapinzani hata kama zitakuwa na uzuri wa namna gani.

Alisema ikiwa Spika ataendelea kuliendesha Bunge kwa kuangalia mtazamo wa chama chake, chombo hicho katika kipindi kilichobaki kufikia uchaguzi wa 2015 kitajishushia heshima mbele ya jamii.

DK. LWAITAMA
Mhadhiri mstaafu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk. Xazaveri Lwaitama, alisema vurugu hizo zilizotokea juzi ni matokeo ya kuwa na Bunge ambalo lina theluthi mbili ya wabunge kutoka chama kimoja.

Alisema Bunge lolote likishakuwa na theluthi mbili ya wabunge kutoka chama kimoja hakuwezi kuwa na ufanisi na ndiyo maana hoja za wabunge wa upinzani ambao ni wachache kila zinapowasilishwa bungeni zinatupwa bila sababu za msingi.

Alitoa mfano kwa matatizo ya maji katika Jiji la Dar es Salaam ambayo ilikuwa hoja ya Mnyika, alisema siyo jambo la kupuuzwa na wabunge wa CCM akiwamo Spika kwa kuwa wao tangu uhuru wameshindwa kuwapatia wananchi huduma hiyo. Alisema katika kipindi cha Uchaguzi Mkuu mwaka 2010, serikali iliweka mabomba ya Wachina na ilipoona upinzani umechukua majimbo ya Kawe na Ubungo, miundombinu hiyo ilitelekezwa hadi sasa bila kutoa maji.

UPINZANI KUWASILISHA HOJA KUMNG'OA SPIKA, NAIBU
Kambi ya Upinzani bungeni imekata rufaa dhidi ya maamuzi yaliyotolewa na Spika wa Bunge, Anne Makinda, bungeni jana na pia dhidi ya hoja za wabunge wa upinzani.

Aidha, kambi hiyo pia itawasilisha hoja ya kumwondoa Spika pamoja na Naibu wake ambayo inatakiwa kuungwa mkono na theluthi moja ya wabunge wote.

Akizungumza na NIPASHE jana, Mnadhimu Mkuu wa kambi hiyo bungeni, Tundu Lissu, alisema rufaa hizo zitawasilishwa kabla ya Ijumaa wiki hii.
Alisema rufaa hizo ni ile ya kupinga uamuzi wa Spika kuiondoa hoja ya mbunge wa Arumeru Mashariki, Joshua Nasari, kuhusu mwenendo wa Baraza la Mitihani la Taifa (Necta), unavyoathiri elimu ya Tanzania.

Alisema rufaa nyingine ni dhidi ya maamuzi ya Naibu Spika, Job Ndugai, kuhusu hoja ya mbunge wa Kuteuliwa (NCCR-Mageuzi), kuhusu udhaifu ulipo katika sekta ya elimu.

Lissu alisema Spika na Naibu wake, wamekuwa wakifanya kazi kwa kukiuka kanuni za Bunge kwa kufanya upendeleo kwa serikali pamoja na Chama Cha Mapinduzi (CCM).

“Ni maamuzi ambayo sisi haturidhiki nayo, tunaona hayafuati kanuni za Bunge ni maamuzi ambayo yanalenga kuikingia kifua serikali na chama chake,” alisema Lissu.

Lissu ambaye pia ni mbunge wa Singida Mashariki (Chadema), alisema kambi ya upinzani imebaini kwamba kiti cha Spika kinafanya kazi kwa upendeleo na kwa chuki dhidi ya wapinzani.
“Spika anatakiwa na kanuni za Bunge kufanyakazi kwa kufuata kanuni, kwa haki, uadilifu bila chuki wala upendeleo wowote...Spika Makinda na Ndugai wameonyesha kwamba hawatendi haki, wanafanya kazi kwa upendeleo na wanatukana wabunge kwamba hawajui kanuni,” alisema.

Hata hivyo, kwa mujibu wa kanuni, rufaa hizo zitawasilishwa kwa spika ambaye ataitisha kikao cha kamati ya kanuni ambayo Mwenyekiti wake ni Spika na Makamu Mwenyekiti ni Naibu Spika.

WABUNGE, WADAU WA SIASA WAANZA KUKUMBUKA BUNGE LA SAMWEL SITTA


UBABE unaolalamikiwa na wabunge wa upinzani dhidi ya Spika wa Bunge, Anne Makinda na Naibu wake, Job Ndugai, umeendelea kupingwa kila kona, huku waziri mwandamizi katika Serikali ya Rais Jakaya Kikwete, naye amejitokeza kupinga namna shughuli za Bunge zinavyoendeshwa.
Baadhi ya wabunge waandamizi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) wamefikia hatua ya kusema kuwa kwa hiki kinachotokea sasa, Makinda na Ndugai wameshusha heshima na hadhi ya Bunge iliyoachwa na Samwel Sitta, aliyejulikana kama Spika wa Kasi na Viwango.
Baadhi ya akina mama wamefikia mahali pa kusema kuwa rekodi mbaya inayowekwa na Makinda bungeni inawaharibia wanawake, hasa wale waliokuwa wanawaza kuwania nafasi za uongozi wa juu, na waliodhani mama huyu angeweza kuwa mfano mwema wa akina mama katika uongozi.
Sambamba na waziri huyo, pia Mwenyekiti wa Taifa wa Chama cha Wananchi (CUF), Prof. Ibrahim Lipumba, amedai wabunge wa CHADEMA hawatumwi na Katibu Mkuu wao, Dk. Willibrod Slaa kufanya vurugu bungeni bali wanatetea haki zao.
Kwa upande wao, baadhi ya wabunge wa CCM waliokataa kutajwa, wamewalalamikia Makinda na Ndugai kuwa uendeshaji wao wa shughuli za Bunge, unawapa sifa wapinzani.
Makada hao wa CCM walisema kuwa hoja binafsi mbili zilizowasilishwa na wabunge wa upinzani na kisha kuondolewa katika mazingira ya kutatanisha, zimewapa sifa zaidi wapinzani.
Akizungumza na Tanzania Daima mjini Dodoma, waziri huyo mwandamizi aliyeomba kuhifadhiwa jina lake, alisema kuwa haungi mkono kiti cha spika kuondoa hoja hizo kwa sababu zozote zile.
"Hoja ya Mnyika ilihusu tatizo la maji jijini Dar es Salaam. Ni tatizo kubwa sana na kila mkazi wa jiji hilo anajua. Ukiiondoa kwa sababu za kukiuka kanuni, mwananchi ambaye hajui kanuni hatakuelewa.
"Mwananchi anajua Mnyika katoa hoja nzito kumaliza tatizo la maji, wabunge wa CCM wamekataa. Haya mengine ya kanuni sijui hoja gani ijadiliwe kwanza, mwananchi haelewi," alisema waziri huyo.
Waziri huyo ambaye ni maarufu kutokana na msimamo wake katika nyadhifa mbalimbali alizowahi kushika, alisema kuondolewa kwa hoja ya Mnyika kuhusu tatizo la maji Dar es Salaam, kumewaweka pabaya sana wabunge wa CCM wa mkoa huo.
Alisema ili CCM ibaki salama na ishinde majimbo ya Mkoa wa Dar es Salaam mwaka 2015, lazima serikali ihakikishe inatekeleza ahadi iliyotoa bungeni wakati wa kujibu hoja ya Mnyika, kwamba ifikapo mwaka 2015, tatizo la maji litakuwa historia katika jiji hilo.
Alipendekeza kuwa ili kiti cha spika kiendeshe mijadala ya hoja binafsi zenye kugusa moja kwa moja matatizo ya wananchi, ni bora akakaa na watoa hoja hata zaidi ya mara tatu kujadiliana nao ili inapokuja bungeni isikwamishwe na kanuni.
Alitahadharisha kuwa wapinzani ni wajanja, kwani hoja wanazoibua zinagusa matatizo halisi ya wananchi, na wabunge wa CCM wanapopingana nao, hawawezi kueleweka.
Kauli ya waziri huyo inaelekeana na ile ya Dk. Slaa aliyoitoa juzi, akidai kuwa kiti cha spika chini ya Makinda kimepwaya kwa maamuzi tofauti na ya wakati ule wa Bunge la Tisa chini ya Spika Samuel Sitta.
“Mimi nasema afadhali ya Sitta mara kumi kuliko huyu Makinda. Sitta alikuwa na aibu ya kupindisha sheria, na ilikuwa ukimbana kwenye hoja anakubaliana na hoja yako kwa manufaa ya Watanzania,” alisema Dk. Slaa.
Naye mmoja wa wabunge wa CCM Mkoa wa Dar es Salaam, alisema  kuondolewa kwa hoja ya Mnyika ni kitanzi kwao.
"Kwenye kikao cha ndani, CCM tulishapanga kukwamisha na kuiondoa hoja ya Mnyika. Lakini kama ingefika hatua ya kuchangiwa, ningechangia kwa ukali zaidi kuishambulia serikali itimize ahadi yake,” alisema bila kutaka kutajwa.
Wiki iliyopita, Mbunge wa Ubungo, Mnyika na wa Arumeru Mashariki, Joshua Nassari (CHADEMA), waliwasilisha hoja binafsi, lakini ziliondolewa.
Mbunge mwingine wa upinzani aliyeleta hoja binafsi ni James Mbatia (NCCR Mageuzi).
Mbatia aliye mbunge wa kuteuliwa na rais, alileta hoja nzito ya udhaifu wa elimu nchini ambayo ilizua mjadala mkubwa.
Hoja ya Mbatia iliyozua mjadala mkubwa bungeni, ilipingwa na wabunge wote wa CCM na baadaye Naibu Spika, Ndugai aliipitisha kibabe huku wabunge wote wa kambi rasmi ya upinzani wakisusia na kutoka nje.
Hoja ya Mnyika ambayo ilihusu uboreshaji wa huduma ya maji katika Jiji la Dar es Salaam, iliondolewa baada ya Waziri wa Maji, Profesa Jumanne Maghembe kuja na hoja ya kutaka iondolewe kwa madai kuwa tayari serikali imetenga sh trilioni 1.8 kwa ajili ya kuboresha huduma na miundombinu ya maji.
Pia alisema hoja hiyo iondolewe kwa vile inazungumzia tatizo la maji katika Jiji la Dar es Salaam wakati tatizo la maji ni la nchi nzima.
Hata hivyo, Mnyika tayari alishafanyia marekebisho hoja yake kwa kuingiza utekelezaji wa miradi ya maji nchi nzima.
Alipanua wigo wa hoja yake kwa kuingiza masuala muhimu kuhusu Programu ya Maji Safi na Mazingira Vijijini (RWSSP), maarufu kama Mradi wa Vijiji Kumi ambao unatekelezwa katika halmashauri za Dar es salaam na wilaya zote nchini.
Nassari alileta hoja kuhusu matatizo yanayolikabili Baraza la Mitihani nchini (NECTA) na kupendekeza marekebisho yake.
Hata hivyo, hoja hiyo iliondolewa kwa kile Spika Makinda alichosema kuwa kukithiri kwa vitendo vya utovu wa nidhamu kwa wabunge wakati wa kujadili hoja hizo binafsi.

Lipumba anena
Mwenyekiti wa CUF, Prof. Lipumba amesema kuwa Katibu Mkuu wa CHADEMA, Dk. Slaa hakuwatuma wabunge wake kufanya vurugu bungeni bali wanafanya hivyo kudai haki zao.
Kauli ya Lipumba inakuja huku kukiwa na upotoshaji unaoenezwa kuwa Dk. Slaa ndiye anachochea vurugu hizo kwa wabunge wake.
Badala yake mwanasiasa huyo alifafanua kuwa wabunge hao walikuwa na haki na kujenga hoja katika madai yao ya msingi, hasa kwa kuwakilisha matatizo ya wananchi wao.
Akizungumza jana na Tanzania Daima jijini Dar es Salaam, katika viwanja vya Mahakama Kuu, Prof. Lipumba alisema kuwa kupindisha hoja binafsi ya Mnyika si haki na maadili ya kiti chao.
Lipumba alisema kuwa kuwapinga wabunge hao na kuziondoa hoja zote binafsi wanazowakilisha kwa ajili ya matatizo ya wananchi si haki, na inaonesha upungufu katika kiti hicho hasa katika kutenda haki.
“Inasikitisha spika na naibu wake hawafuati utaratibu ndiyo maana sisi CUF tumependekeza katika katiba mpya spika asiwe mbunge,” alisema.
Siku mbili zilizopita, Bunge lililazimika kuahirisha vikao kabla ya muda wake kutokana na kutoelewana kwa wabunge wa upinzani, kiti cha spika na serikali kwa upande mwingine, wakati wa kujadili na kupitisha hoja binafsi za wabunge.
Naye Mwenyekiti wa Jukwaa la Katiba, Deus Kibamba, alisema kuwa inasikitisha Bunge kuwa na hali hiyo wakati hoja binafsi inatakiwa iheshimiwe.
Alisema kuwa kuzuia hoja binafsi ya mbunge si jambo jema na kumtaka Naibu Spika, Ndugai kutumia hekima badala ya msuli.
“Kutumia msuli haifai, na kinachoonekana dhahiri alipania kufifisha hoja ya upinzani. Kiti cha spika kinataka mtu mwenye busara na hekima, yaani imeonekana kuwa kiti hicho kinakwamisha hoja za upinzani,” alisema