Sunday, February 17, 2013

Spika akaliwa kooni

Spika akaliwa kooni


Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kimetangaza kwenda kwa wananchi ambao wanaunda mahakama iliyo kubwa kuliko zote nchini kwa nia ya kuwapelekea hoja binafsi zenye maslahi kwa taifa zilizozimwa nje ya utaratibu na kiti cha Spika.

Aidha, Chadema kimewaelekeza wabunge wake wote watakaoitwa na Kamati ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge, wasiende kuhojiwa kama alivyoelekeza Spika wa Bunge, Anne Makinda.

Msimamo huo ulitangazwa jana jijini Dar es Salaam na Katibu Mkuu wa Chadema, Dk. Willibrod Slaa, kwa waandishi wa habari na kufafanua kuwa wabunge wa chama chake wameelekezwa wasiende kuhojiwa kutokana na kiti cha Spika kuonyesha upendeleo wa wazi kwa serikali dhidi ya hoja binafsi za wabunge.

Hoja zilizokataliwa ni ya Mbunge wa Kuteuliwa, James Mbatia kuhusu udhaifu katika mitaala na hoja ya Mbunge wa Ubungo (Chadema), John Mnyika, iliyohusu matatizo ya maji katika Jiji la Dar es Salaam.

Hoja ya Mbatia ilikataliwa Ijumaa iliyopita na kuwalazimisha wabunge wote wa upinzani kutoka nje ya ukumbi wa Bunge wakati hoja ya Mnyika ilikataliwa juzi na kusababisha mvutano bungeni kati ya serikali na wabunge wa CCM kwa upande mmoja na wale wa upinzani kwa upande mwingine na kumlazimisha Naibu Spika Ndugai, kuahirisha kikao.

Dk. Slaa alisema wabunge wa Chadema wametakiwa kutoitikia wito wa kuhojiwa na Kamati hiyo inayoongozwa na Mbunge wa Mlalo (CCM), Brigedia Jenerali mstaafu Hassan Ngwilizi, hadi pale rufaa 10 zilizokatwa na wabunge wa Chadema kwa nyakati tofauti zitakapotolewa maamuzi.

KWENDA KWA WANANCHI
Akizungumzia suala la kwenda kwa wananchi, Dk. Slaa alisema kuwa hatua hiyo imechukuliwa na chama hicho baada ya kuona kwamba Bunge ambalo ni chombo pekee kikuu nchini kwa mujibu wa Ibara ya 63 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania chenye wajibu wa kuisimamia serikali kugeuzwa na viongozi wake kuwa sehemu ya serikali.

“Na ndiyo maana unaona sasa Spika anatumika kupindisha kanuni za Bunge kwa minajili ya kutimiza matakwa ya serikali na hivyo kuonyesha kwamba yupo pale kwa manufaa ya serikali kinyume cha kanuni ya nane ya Bunge,” alisema.

Alisema Chadema kama chama makini, hakiwezi kukaa kimya na kuona Bunge ambalo ndilo chombo kitakatifu zaidi hata ya Ikulu kwa sababu linawakilisha wananchi, linageuzwa kuwa ‘komedi’ kwa kuzima hoja binafsi za wabunge kama ya Mnyika na Mbatia na hivyo kufanya Bunge kutokuwa na tija, zaidi ya kuteketeza mamilioni ya fedha za wananchi.

Alisema Mkutano wa Bunge unaoendelea sasa unagharimu zaidi ya Shilingi bilioni moja na  alitarajia fedha hizo zitumike kuhalalisha mijadala na maamuzi yenye tija tofauti ilivyofanyika safari hii.

Akizungumzia uamuzi wa kuwazuia wabunge wao kutoitikia wito wa kamati ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge, kama kilivyoelekeza kiti cha Spika mpaka pale maamuzi ya rufaa zote kumi zilizokatwa na wabunge wa chama chake zilizoko kwa Spika yatakapotolewa bungeni na tena hadharani.

  Dk. Slaa alisema wamefikia hatua hiyo kwa misingi kuwa Spika ambaye anayepaswa kusimamia kanuni, ndiye amekuwa wa kwanza kuzivunja.

“Kati ya rufaa hizo kumi alizozikalia Spika, nitaje mbili kwa faida ya wananchi, moja ni ile ya Godbless Lema (Mbunge wa Arusha Mjini (Chadema) aliyetakiwa kuthibitisha tuhuma kwamba Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, alilidanganya Bunge na alipeleka ushahidi na Spika akaukalia hadi leo,” alisema.

Dk. Slaa alitaja pia ushahidi alioutoa Mbunge wa Singida Mashariki (Chadema), Tundu Lissu, kuhusiana na tuhuma za kuteuliwa majaji wasio na sifa na alithibitisha kwa vielelezo alivyovipeleka kwa Spika ikiwa ni pamoja na kumtaja jina jaji mmoja wa Mahakama ya Rufaa, lakini juhudi zake zote zimeishia kwenye mikono ya Spika.

Dk. Slaa aliwaasa Watanzania wanapokwenda kwenye mabaraza ya katiba kuhakikisha wanajenga hoja zitakazozuia Spika kupatikana kutoka kwenye chama cha siasa, badala yake wapendekeze Spika kupatikana kutokana na sifa maalum kama za elimu na kupitia kwenye uhakiki wa chombo maalum kitakachopendekezwa kwa ajili ya kufanya kazi hiyo.


NGWILIZI AKABIDHIWA JUKUMU
Kamati  ya Uongozi ya Bunge imepeleka sakata la vurugu zilizotokea juzi jioni katika Kamati ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge, ili ilichunguze na kutoa mapendekezo bungeni kabla ya Mkutano wa 10 kumalizika.

Aidha, kamati hiyo imesimamisha uwasilishaji wa hoja binafsi zilizopangwa kuwasilishwa na wabunge katika mkutano huu.

Vurugu hizo zilitokea juzi baada ya Waziri wa Maji, Profesa Jumanne Maghembe, kuwasilisha hoja ya kutaka hoja ya Mnyika iondolewe.

Akizungumza mara baada ya kipindi cha maswali na majibu bungeni jana, Spika Makinda, alisema maamuzi hayo yalifikiwa juzi katika kikao cha dharura cha kamati ya Uongozi.
“Kamati ilikubaliana kuwa hoja zote binafsi za wabunge zisiwasilishwe bungeni kutokana na utovu wa nidhamu uliokuwa umeanza ili kuzuia mwendelezo ambao ungeweza kujitokeza katika hoja binafsi zilizobakia kwa kulinda heshima ya Bunge,” alisema na kuongeza:

“Kamati ilikemea kwa nguvu zote vitendo hivyo na kubainisha kwamba endapo vitaachiwa viendelee vinaweza kusababisha madhara makubwa kama kupigana ndani ya Bunge.”

Kuhusu uamuzi wa kusitisha hoja binafsi, Spika Makinda alisema imelazimu Bunge  kuahirisha mijadala ya Hoja Binafsi kutokana na tabia iliyojitokeza ya utovu wa nidhamu kwa baadhi ya Wabunge.

Alisema wabunge hao waliamua  kwa makusudi kuanzisha vurugu na hivyo kulifanya Bunge lianze kupoteza heshima yake ya Kibunge.

“Waheshimiwa wabunge, siku zote nimekuwa nikisisitiza matumizi ya Kanuni za Bunge ambazo ndizo mwongozo wa uendeshaji wa Bunge.  Hoja Binafsi za wabunge zinaongozwa na Kanuni za Bunge kuanzia Kanuni ya 53 hadi 58 na Kanuni za majadiliano zinaongozwa na Kanuni kuanzia 59 hadi 71 ambazo kwa ujumla wake zikifuatwa kama inavyotakiwa, vurugu haiwezi kutokea Bungeni,” alisema.

Alisema katika mkutano huu ambao unatarajiwa kumalizika Ijumaa,  imeonyesha waziwazi baadhi ya wabunge kwa makusudi na kwa nia ya kupotosha wananchi wakitumia vibaya kanuni hizo na wakati mwingine kuwadanganya wananchi ambao kwa bahati mbaya hawazifahamu kanuni au hazifuatwi na kiti ama zinakiukwa.

“Waheshimiwa Wabunge, kwa masikitiko makubwa sote tulishuhudia vurugu zilizojitokeza katika Bunge hili hasa wakati wa mjadala wa hoja binafsi za wabunge, kimsingi huu ulikuwa ni utovu wa nidhamu wa hali ya juu kutokea katika Historia ya Bunge letu,” alisema na kuongeza:

“Taasisi ya Bunge inalaani vitendo vilivyojitokeza jana (juzi) vilivyovunja Kanuni ya 60(2) inayokataza Mbunge kuzungumza kabla ya kuruhusiwa na Spika na Kanuni ya 60(12) inayowataka Wabunge kukaa chini wakati wowote Spika anaposimama kutaka kuzungumza.”
Aidha, alisema kumekuwa kuna madai kuwa Kiti kinatoa upendeleo wa wazi kwa Serikali dhidi ya Upinzani, jambo ambalo si kweli.

Hata hivyo, alisema  kama maamuzi yanayofanywa na Kiti yana kasoro kanuni zinaruhusu mbunge ambaye hakuridhika na maamuzi hayo, kukata rufaa kwenye Kamati ya Kanuni za Bunge kwa mujibu wa Kanuni ya 5 (4).

Alisema  vitendo vya uvunjifu wa Kanuni na kusababisha fujo kumedhalilisha Kiti na Taasisi ya Bunge kwa ujumla.

Akizungumzia kuhusiana na kuondolewa kwa hoja ya Mnyika, Makinda alisema hoja hiyo ilikidhi vigezo na alipewa nafasi ya kuiwasilisha Bungeni na akawasilisha hoja yake.
Alisema baada ya Hoja hiyo kuwasilishwa, kwa mujibu wa kanuni ya 53(6) (c) Waziri wa Maji ambaye ndiye msemaji wa Serikali kuhusu maudhui ya Hoja husika, alipewa nafasi ya kuwa mchangiaji wa kwanza na kutoa maoni ya shughuli za Serikali juu ya hoja ya Mnyika.

‘KITI CHA SPIKA KINAYUMBA’
Baadhi ya watu wamesema Spika Makinda na Naibu wake. Job Ndugai  ndiyo chanzo cha kuvuruga Bunge na kusababisha heshima yake kushuka mbele ya Watanzania.

DEUS KIBAMBA
Mwenyekiti wa Jukwaa la Katiba Tanzania, Deus Kibamba, alimkumbuka Spika aliyepita, Samel Sitta, na kusema kuwa alikuwa anatenda haki na ndiyo maana wabunge wengi walikuwa wanamheshimu na hapakuwa na vurugu kama za sasa.

Alisema ili kulipa Bunge heshima yake inayostahili, ni lazima kila hoja binafsi inayowasilishwa iheshimiwe na mbunge aliyeiwasilisha apewe heshima yake.

Alimtaka Spika kuacha utaratibu wa kufanya kazi kwa kuangalia itikadi za chama.
Alisema hoja za wapinzani ambazo wamekuwa wakiziwasilisha bungeni zimekuwa na maana, lakini wabunge wa CCM pamoja na Spika wamekuwa wakiziponda bila sababu na kutaka ziondolewe mezani.

“Hoja hizi za wapinzani zimekuwa zikiwapa changamoto wabunge wa CCM,  ingawa wamekuwa wakiziona kama hazina maana,” alisema Kibamba.
RAIS TLS

Rais wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS), Francis Sitolla, alisema kuna udhaifu mkubwa katika kuwadhibiti wabunge na kuwaelekeza wanapokuwa wanajadili hoja mbalimbali.
Alisema ni dhahiri kwamba kiti cha Spika kinayumba kutokana na kuonekana wazi kwamba anaendesha Bunge kwa upendeleo huku akiwanyima wapinzani haki.

Aliongeza kuwa kiti cha Spika kama mwamuzi huru, kinatakiwa kutenda haki kwa kila upande ili jamii na wabunge waweze kukiamini hususani inapozuka mijadala mikali.

Alisema matatizo ya kumchagua Spika anayetokana na chama cha siasa kwa sasa yameanza kujitokeza na kwamba hali hiyo inaweza kuwa mbaya katika kipindi kilichobaki kabla ya Uchaguzi Mkuu mwaka 2015.

Aidha, Stolla aliwataka wabunge kwa upande mwingine kuwa wavumilivu pale hoja zinapojadiliwa, lakini alisema hilo litaweza kufanyika kama wataamini wanatendewa haki ndani ya Bunge.

“Spika siyo tu aonekane ametenda haki kwa wabunge wa upinzani bali haki lazima ionekane imetendeka na hapo ndipo anaweza kuaminiwa na pande zote,” alisema Stolla.

HELLEN KIJO-BISIMBA

Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu, Dk. Hellen Kijo-Bisimba, alisema vurugu za juzi bungeni zilitokana na kiti cha Spika kuvaa miwani ya kuona upande mmoja na  kwamba huo ni udhaifu mkubwa.

Dk. Bisimba alisema Bunge limeshindwa kuangalia shida mbalimbali zinazowakabili Watanzania badala yake limejikita kukwamisha hoja za wapinzani hata kama zitakuwa na uzuri wa namna gani.

Alisema ikiwa Spika ataendelea kuliendesha Bunge kwa kuangalia mtazamo wa chama chake, chombo hicho katika kipindi kilichobaki kufikia uchaguzi wa 2015 kitajishushia heshima mbele ya jamii.

DK. LWAITAMA
Mhadhiri mstaafu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk. Xazaveri Lwaitama, alisema vurugu hizo zilizotokea juzi ni matokeo ya kuwa na Bunge ambalo lina theluthi mbili ya wabunge kutoka chama kimoja.

Alisema Bunge lolote likishakuwa na theluthi mbili ya wabunge kutoka chama kimoja hakuwezi kuwa na ufanisi na ndiyo maana hoja za wabunge wa upinzani ambao ni wachache kila zinapowasilishwa bungeni zinatupwa bila sababu za msingi.

Alitoa mfano kwa matatizo ya maji katika Jiji la Dar es Salaam ambayo ilikuwa hoja ya Mnyika, alisema siyo jambo la kupuuzwa na wabunge wa CCM akiwamo Spika kwa kuwa wao tangu uhuru wameshindwa kuwapatia wananchi huduma hiyo. Alisema katika kipindi cha Uchaguzi Mkuu mwaka 2010, serikali iliweka mabomba ya Wachina na ilipoona upinzani umechukua majimbo ya Kawe na Ubungo, miundombinu hiyo ilitelekezwa hadi sasa bila kutoa maji.

UPINZANI KUWASILISHA HOJA KUMNG'OA SPIKA, NAIBU
Kambi ya Upinzani bungeni imekata rufaa dhidi ya maamuzi yaliyotolewa na Spika wa Bunge, Anne Makinda, bungeni jana na pia dhidi ya hoja za wabunge wa upinzani.

Aidha, kambi hiyo pia itawasilisha hoja ya kumwondoa Spika pamoja na Naibu wake ambayo inatakiwa kuungwa mkono na theluthi moja ya wabunge wote.

Akizungumza na NIPASHE jana, Mnadhimu Mkuu wa kambi hiyo bungeni, Tundu Lissu, alisema rufaa hizo zitawasilishwa kabla ya Ijumaa wiki hii.
Alisema rufaa hizo ni ile ya kupinga uamuzi wa Spika kuiondoa hoja ya mbunge wa Arumeru Mashariki, Joshua Nasari, kuhusu mwenendo wa Baraza la Mitihani la Taifa (Necta), unavyoathiri elimu ya Tanzania.

Alisema rufaa nyingine ni dhidi ya maamuzi ya Naibu Spika, Job Ndugai, kuhusu hoja ya mbunge wa Kuteuliwa (NCCR-Mageuzi), kuhusu udhaifu ulipo katika sekta ya elimu.

Lissu alisema Spika na Naibu wake, wamekuwa wakifanya kazi kwa kukiuka kanuni za Bunge kwa kufanya upendeleo kwa serikali pamoja na Chama Cha Mapinduzi (CCM).

“Ni maamuzi ambayo sisi haturidhiki nayo, tunaona hayafuati kanuni za Bunge ni maamuzi ambayo yanalenga kuikingia kifua serikali na chama chake,” alisema Lissu.

Lissu ambaye pia ni mbunge wa Singida Mashariki (Chadema), alisema kambi ya upinzani imebaini kwamba kiti cha Spika kinafanya kazi kwa upendeleo na kwa chuki dhidi ya wapinzani.
“Spika anatakiwa na kanuni za Bunge kufanyakazi kwa kufuata kanuni, kwa haki, uadilifu bila chuki wala upendeleo wowote...Spika Makinda na Ndugai wameonyesha kwamba hawatendi haki, wanafanya kazi kwa upendeleo na wanatukana wabunge kwamba hawajui kanuni,” alisema.

Hata hivyo, kwa mujibu wa kanuni, rufaa hizo zitawasilishwa kwa spika ambaye ataitisha kikao cha kamati ya kanuni ambayo Mwenyekiti wake ni Spika na Makamu Mwenyekiti ni Naibu Spika.

No comments:

Post a Comment