UBABE unaolalamikiwa na
wabunge wa upinzani dhidi ya Spika wa Bunge, Anne Makinda na Naibu wake,
Job Ndugai, umeendelea kupingwa kila kona, huku waziri mwandamizi
katika Serikali ya Rais Jakaya Kikwete, naye amejitokeza kupinga namna
shughuli za Bunge zinavyoendeshwa.
Baadhi ya wabunge
waandamizi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) wamefikia hatua ya kusema kuwa
kwa hiki kinachotokea sasa, Makinda na Ndugai wameshusha heshima na
hadhi ya Bunge iliyoachwa na Samwel Sitta, aliyejulikana kama Spika wa
Kasi na Viwango.
Baadhi ya akina mama
wamefikia mahali pa kusema kuwa rekodi mbaya inayowekwa na Makinda
bungeni inawaharibia wanawake, hasa wale waliokuwa wanawaza kuwania
nafasi za uongozi wa juu, na waliodhani mama huyu angeweza kuwa mfano
mwema wa akina mama katika uongozi.
Sambamba na waziri huyo,
pia Mwenyekiti wa Taifa wa Chama cha Wananchi (CUF), Prof. Ibrahim
Lipumba, amedai wabunge wa CHADEMA hawatumwi na Katibu Mkuu wao, Dk.
Willibrod Slaa kufanya vurugu bungeni bali wanatetea haki zao.
Kwa upande wao, baadhi
ya wabunge wa CCM waliokataa kutajwa, wamewalalamikia Makinda na Ndugai
kuwa uendeshaji wao wa shughuli za Bunge, unawapa sifa wapinzani.
Makada hao wa CCM
walisema kuwa hoja binafsi mbili zilizowasilishwa na wabunge wa upinzani
na kisha kuondolewa katika mazingira ya kutatanisha, zimewapa sifa
zaidi wapinzani.
Akizungumza na Tanzania
Daima mjini Dodoma, waziri huyo mwandamizi aliyeomba kuhifadhiwa jina
lake, alisema kuwa haungi mkono kiti cha spika kuondoa hoja hizo kwa
sababu zozote zile.
"Hoja ya Mnyika ilihusu
tatizo la maji jijini Dar es Salaam. Ni tatizo kubwa sana na kila mkazi
wa jiji hilo anajua. Ukiiondoa kwa sababu za kukiuka kanuni, mwananchi
ambaye hajui kanuni hatakuelewa.
"Mwananchi anajua Mnyika
katoa hoja nzito kumaliza tatizo la maji, wabunge wa CCM wamekataa.
Haya mengine ya kanuni sijui hoja gani ijadiliwe kwanza, mwananchi
haelewi," alisema waziri huyo.
Waziri huyo ambaye ni
maarufu kutokana na msimamo wake katika nyadhifa mbalimbali alizowahi
kushika, alisema kuondolewa kwa hoja ya Mnyika kuhusu tatizo la maji Dar
es Salaam, kumewaweka pabaya sana wabunge wa CCM wa mkoa huo.
Alisema ili CCM ibaki
salama na ishinde majimbo ya Mkoa wa Dar es Salaam mwaka 2015, lazima
serikali ihakikishe inatekeleza ahadi iliyotoa bungeni wakati wa kujibu
hoja ya Mnyika, kwamba ifikapo mwaka 2015, tatizo la maji litakuwa
historia katika jiji hilo.
Alipendekeza kuwa ili
kiti cha spika kiendeshe mijadala ya hoja binafsi zenye kugusa moja kwa
moja matatizo ya wananchi, ni bora akakaa na watoa hoja hata zaidi ya
mara tatu kujadiliana nao ili inapokuja bungeni isikwamishwe na kanuni.
Alitahadharisha kuwa
wapinzani ni wajanja, kwani hoja wanazoibua zinagusa matatizo halisi ya
wananchi, na wabunge wa CCM wanapopingana nao, hawawezi kueleweka.
Kauli ya waziri huyo
inaelekeana na ile ya Dk. Slaa aliyoitoa juzi, akidai kuwa kiti cha
spika chini ya Makinda kimepwaya kwa maamuzi tofauti na ya wakati ule wa
Bunge la Tisa chini ya Spika Samuel Sitta.
“Mimi nasema afadhali ya
Sitta mara kumi kuliko huyu Makinda. Sitta alikuwa na aibu ya
kupindisha sheria, na ilikuwa ukimbana kwenye hoja anakubaliana na hoja
yako kwa manufaa ya Watanzania,” alisema Dk. Slaa.
Naye mmoja wa wabunge wa CCM Mkoa wa Dar es Salaam, alisema kuondolewa kwa hoja ya Mnyika ni kitanzi kwao.
"Kwenye
kikao cha ndani, CCM tulishapanga kukwamisha na kuiondoa hoja ya
Mnyika. Lakini kama ingefika hatua ya kuchangiwa, ningechangia kwa ukali
zaidi kuishambulia serikali itimize ahadi yake,” alisema bila kutaka
kutajwa.
Wiki
iliyopita, Mbunge wa Ubungo, Mnyika na wa Arumeru Mashariki, Joshua
Nassari (CHADEMA), waliwasilisha hoja binafsi, lakini ziliondolewa.
Mbunge mwingine wa upinzani aliyeleta hoja binafsi ni James Mbatia (NCCR Mageuzi).
Mbatia aliye mbunge wa kuteuliwa na rais, alileta hoja nzito ya udhaifu wa elimu nchini ambayo ilizua mjadala mkubwa.
Hoja
ya Mbatia iliyozua mjadala mkubwa bungeni, ilipingwa na wabunge wote wa
CCM na baadaye Naibu Spika, Ndugai aliipitisha kibabe huku wabunge wote
wa kambi rasmi ya upinzani wakisusia na kutoka nje.
Hoja
ya Mnyika ambayo ilihusu uboreshaji wa huduma ya maji katika Jiji la
Dar es Salaam, iliondolewa baada ya Waziri wa Maji, Profesa Jumanne
Maghembe kuja na hoja ya kutaka iondolewe kwa madai kuwa tayari serikali
imetenga sh trilioni 1.8 kwa ajili ya kuboresha huduma na miundombinu
ya maji.
Pia alisema hoja hiyo
iondolewe kwa vile inazungumzia tatizo la maji katika Jiji la Dar es
Salaam wakati tatizo la maji ni la nchi nzima.
Hata hivyo, Mnyika tayari alishafanyia marekebisho hoja yake kwa kuingiza utekelezaji wa miradi ya maji nchi nzima.
Alipanua wigo wa hoja
yake kwa kuingiza masuala muhimu kuhusu Programu ya Maji Safi na
Mazingira Vijijini (RWSSP), maarufu kama Mradi wa Vijiji Kumi ambao
unatekelezwa katika halmashauri za Dar es salaam na wilaya zote nchini.
Nassari alileta hoja kuhusu matatizo yanayolikabili Baraza la Mitihani nchini (NECTA) na kupendekeza marekebisho yake.
Hata hivyo, hoja hiyo
iliondolewa kwa kile Spika Makinda alichosema kuwa kukithiri kwa vitendo
vya utovu wa nidhamu kwa wabunge wakati wa kujadili hoja hizo binafsi.
Lipumba anena
Mwenyekiti wa CUF, Prof.
Lipumba amesema kuwa Katibu Mkuu wa CHADEMA, Dk. Slaa hakuwatuma
wabunge wake kufanya vurugu bungeni bali wanafanya hivyo kudai haki zao.
Kauli ya Lipumba inakuja huku kukiwa na upotoshaji unaoenezwa kuwa Dk. Slaa ndiye anachochea vurugu hizo kwa wabunge wake.
Badala yake mwanasiasa
huyo alifafanua kuwa wabunge hao walikuwa na haki na kujenga hoja katika
madai yao ya msingi, hasa kwa kuwakilisha matatizo ya wananchi wao.
Akizungumza jana na
Tanzania Daima jijini Dar es Salaam, katika viwanja vya Mahakama Kuu,
Prof. Lipumba alisema kuwa kupindisha hoja binafsi ya Mnyika si haki na
maadili ya kiti chao.
Lipumba alisema kuwa
kuwapinga wabunge hao na kuziondoa hoja zote binafsi wanazowakilisha kwa
ajili ya matatizo ya wananchi si haki, na inaonesha upungufu katika
kiti hicho hasa katika kutenda haki.
“Inasikitisha spika na
naibu wake hawafuati utaratibu ndiyo maana sisi CUF tumependekeza katika
katiba mpya spika asiwe mbunge,” alisema.
Siku mbili zilizopita,
Bunge lililazimika kuahirisha vikao kabla ya muda wake kutokana na
kutoelewana kwa wabunge wa upinzani, kiti cha spika na serikali kwa
upande mwingine, wakati wa kujadili na kupitisha hoja binafsi za
wabunge.
Naye Mwenyekiti wa
Jukwaa la Katiba, Deus Kibamba, alisema kuwa inasikitisha Bunge kuwa na
hali hiyo wakati hoja binafsi inatakiwa iheshimiwe.
Alisema kuwa kuzuia hoja binafsi ya mbunge si jambo jema na kumtaka Naibu Spika, Ndugai kutumia hekima badala ya msuli.
“Kutumia msuli haifai,
na kinachoonekana dhahiri alipania kufifisha hoja ya upinzani. Kiti cha
spika kinataka mtu mwenye busara na hekima, yaani imeonekana kuwa kiti
hicho kinakwamisha hoja za upinzani,” alisema
No comments:
Post a Comment