Padre Ambros Mkenda wa Zanzibar apigwa risasi
Father Ambros Mkenda wa
Kanisa la Katoliki la Mpendae amepigwa risasi na watu wasiojulikana nje
ya nyumba yake majira ya saa 12 jioni leo wakati akitokea kanisani.
Kamanda wa polisi wa Mkoa wa Mjini Magharibi Azizi Juma amethibisha
kutokea kwa tukio hilo na amesema hakuna mtu anayeshikiliwa kuhusika na
tukio hilo lakini uchunguzi unaendelea. Father Mkenda hivi sasa
anapatiwa matibabu katika hospitali ya Mnazi Mmoja, ambapo Askofu wa
Anglikan Michael Hafidh amesema bado ni mapema mno kuelezea kama
ataendelea kuwepo hospitalini hapo au atasafirishwa huku akilaani
vitendo ambavyo hivi vinavyoendelea vya kuwahujumu viongozi wa dini.
(picha: Salma Said)
Watu
wasiojulikana leo wamempiga risasi Father, Ambros Mkenda wa Kanisa
Katoliki la Mpendae Mjini Zanzibar nje ya nyumba yake majira ya saa 12
jioni wakati akitokea Kanisani.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Mjini
Magharibi Aziz Juma Mohammed amethibitisha kutokea kwa tukio hilo ambalo
alisema Father amepigwa risasi na ameumizwa sehemu ya kichwa na amekuwa
akitoka damu nyingi kichwani na tayari anapatiwa matibabu katika
hospitali kuu ya Mnazi Mmoja.
Alisema jeshi la polisi linaendelea na
uchunguzi wa tukio hilo ili kubaini wahusika walifanya uhalifu huo kwa
madhumuni gani kabla ya kuchukuliwa hatua za kisheria.
“Sisi tunahesabu kuwa kitendo hiki ni
kitendo cha kihalifu na tunawatafuta wahalifu waliofanya kitendo hiki
kwa hivyo bado ni mapema kusema kwamba kitendo hiki kimefanywa na nani
kwa kuwa bado uchunguzi wetu unaendelea na hadi sasa hakuna mtu
tuliyemshika kuhusikana na tukio hili” alisema Kamanda.
Kamanda Aziz akisimulia tukio hilo
alisema walipata taarifa majira ya saa 2 na kwenda katika eneo la tukio
ambapo Father alikuwa akitokea kanisani na kutaka kuelekea nyumbani
kwake wakati akiwa ndani ya gari ndipo aliposhambuliwa na watu
wasiojulikana na kuanguka.
“Tumekuta mabaki ya risasi ndani ya gari
yake na katika vioo vyake vya gari vimevunjika na tumekuta damu chini
pale” alisema Kamanda.
Aidha Kamanda Azizi alisema Father
Ambros yeye ni mhasibu pale kanisani na hivyo mara nyingi watu
wananaamini kwamba katika siku za krismass mara nyingi sadaka hukusanywa
fedha nyingi na hivyo wanamini kwamba alikuwa fedha mikononi na ndipo
inawezekana waliamua kumpiga risasi wakitaka kuchukua fedha hizo.
Hata hivyo alisema uchunguzi wa awali
ndio utakaoeleza ni suala gani lililopelekea kupigwa risasi lakini
wanaendelea na uchunguzi huo ambapo uchunguzi ndio utakaojulikana sababu
kamili ya tukio hilo.
Akizungumzia tukio hilo, Askofu Michael
Hafidh wa Kanisa la Anglikan la Mkunazini amesema wamesikitishwa na
wamepokea kwa mshituko mkubwa tukio hilo hasa kwa kuzingatia matukio
kama hayo hayajawahi kutokea ya kuwahujumu viongozi wa dini.
Alisema tukio hilo ni miongoni mwa
matukio ya kushtusha na yanaashiria hali mbaya ya kiusalama na kuwaomba
viongozi wa serikali kuchukua hatua za tahadhari kubwa kwani matukio
kama hayo yameanza kutokea kwa viongozi wa dini ambapo mwanzo ilianzia
kwa Sheikh Soraga na baadae kutokea kwa Father Ambros.
“Hii ni hali ya hatari katika nchi yetu
na haipendezi lakini serikali lazima ijue sisi hatuwezi kujua wala
hatuwezi kujilinda lakini serikali inapaswa kutulinda sisi ndio wananchi
wake” alisema Askofu Hafidh.
Askofu Hafidh alisema hivi karibuni
kumekuwepo vipeperushi vilivyosambazwa na watu vikiwatisha watu wenye
imani ya kikristo ambapo alisema miongoni mwao walikuwa na khofu juu ya
kusambazwa kwa vipeperushi hivyo na kuiomba serikali iongeze ulinzi.
“Tumeona hivi vipeperushi na kwa kweli
tulikuwa na khofu juu ya vipeperushi hivi lakini ndio tunasema
tunaelekea wapi katika maisha haya,” alisema Akofu Hafidh.
“Sisi hatuamini kwamba kuna kisasi kwa
viongozi wa dini lakini tunachukulia hilo ni tukio la kihalifu na pia
hatuna vipeperushi vya aina yoyote vinavyoelezea kuwatisha viongozi wa
dini kwa hivyo tunachukulia hayo ni matukio ya kihalifu na wala
hatuamini kwamba matukio haya ni ya dini fulani,” alisema Kamanda Azizi.
Akielezea kuhusiana na hilo Kamanda Aziz
alisema jeshi la polisi limejipanga na kuzidisha ulinzi katika maeneo
yote ya makanisa ambapo kumesambazwa polisi wa kutosha kwa kuwa wanajua
wakati wa sherehe mambo ya kihalifu hujitokeza.
“Sisi kawaida huwa tunaweka ulinzi siku
za sherehe zozote lakini kwanza makanisa yote yamewekwa ulinzi wa
kutosha kabisa lakini wahalifu wanapotaka kufanya uhalifu huwezi kujua
watatumia mbinu gani na saa ngapi na watafanya uhalifu huo wapi, lakini
ulinzi upo wa kutosha,” alisisitiza Kamanda Aziz.
No comments:
Post a Comment